Iringa. Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amepiga marufuku wafugaji kuingiza mifugo yao wilayani humo bila kibali na kuonya kuwa atakayekaidi amri hiyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Pia, amewataka maofisa watendaji kusimamia amri hiyo la sivyo atakayeshindwa au kuhusika kuingiza mifugo isiyo na kibali atawajibishwa.
Kasesela alitoa amri hiyo juzi wakati akifunga mafunzo ya wafugaji 35 wa ng’ombe wa maziwa kutoka mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya katika Ukumbi wa mikutano wa Kiwanda cha Maziwa cha Asas Diaries LTD kilichopo mjini Iringa.
Kasesela alisema umefika wakati kwa wafugaji kuanza kufikiria ufugaji wa kibiashara huku wakizingatia kuwa na mifugo michache yenye kutoa maziwa mengi ili waweze kunufaika nayo.
“Nawasihi mtumie mafunzo mliyoyapata hapa vizuri ili muweze kunufaika kiuchumi, lakini anzeni kufikiria kufuga kibishara kwa kuwa na mifugo michache yenye kuleta faida,” alisema na kuongeza:
“Kwa upande wetu serikalini, tumejipanga kuhakikisha tunahamasisha kila mfugaji kuwa na ranchi ya kuhifadhi mifugo yake na eneo la kulima majani kwa ajili ya malisho, hatutaruhusu mifugo kuzurura,” alisema Kasesela.
Awali, akizungumza kwenye mafunzo hayo, Meneja ununuzi wa kiwanda cha kusindika bidhaa za maziwa cha Asas Diaries Ltd, Roy Omulo aliiomba Serikali kuajiri maofisa ugani kwa wingi ili kusaidia kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji na kuachana na kilimo cha mazoea.
Alisema ukosefu wa maofisa ugani vijijini ndiyo chanzo cha wakulima na wafugaji kufanya shughuli zao kwa mazoea badala ya kufuata utaratibu na kanuni za kilimo na ufugaji bora wa kisasa.
Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, Ashura Gosbert alisema anamiliki ng’ombe wawili ambao hawampatii faida zaidi ya kumpa lita nne ya maziwa ambayo hawezi kuyauza katika kiwanda kikubwa. “Kupitia mafunzo haya nina imani yatanisaidia na ninajiandaa kukabiliana na changamoto ili niongeze uzalishaji na nifikie kiwango cha kuuza maziwa kiwandani,” alisema Ashura.
Mkurugenzi wa Asas, Ahmed Abri alisema kiwanda hicho kilianza kusindika maziwa kati ya lita 1,000 hadi 1,500 kwa kutengeneza maziwa mgando na maziwa halisi baada ya kuona bidhaa hizo zinahitajiwa na watu wengi nchini.
Abri alisema Shirika la Afya Duniani (WHO), linasisitiza kila binadamu anywe maziwa lita 200 kwa mwaka, lakini Watanzania hawafikishi hata lita 10 kwa kipindi hicho.
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT