NENO LA MUNGU:UNYENYEKEVU NDIO NGUZO KUU PEKEE YA KUMUONA MUNGU.
SOMA HATA MWISHO;
BWANA YESU KRISTO ASIFIWE MPENDWA,
Natumai umekuwa na wakati mwema,binafsi namshukuru Mungu Mkuu wa yote kwa uhai,sasa tupitie ujumbe huu ambao Roho Wa Mungu ananiongoza niutoe wakati huu,mistari ya Kitabu cha Zaburi ambayo leo tunapitia mistari yake michache ya Mlango wa 51,inatuonyesha namna ya kutubu,kutubu maana yake unakubali kuwa umekosa na wewe ni mkosa na unaomba msamaha wa kweli pasipo kuyarejelea makosa.
Tutapitia pia mistari mingine ya vitabu vingine kadri Roho atakavyo niongoza,KARIBU tuambatane pamoja kuzijenga Roho zetu kwa chakula hichi toka kwa Mungu.
Katika jambo linalomchukiza Mungu ni kitu kinaitwa KIBURI,nadhani utakumbuka Mfalme Farao wa Misri na Mfalme Nebukadreza au waweza mwiita Nebukadneza huyo naye alikuwa Mfalme wa Babeli,walipoweka KIBURI katika maagizo aliyotoa Mungu kupitia Watumishi wake juu ya wana wa Israeli kutolewa utumwani,Mungu aliwaonyesha kwamba Yeye ni Mungu Aliye Hai,Farao alipewa mapigo kumi,huku Nebukadreza akitolewa kwenye nyumba ya Kifalme hadi msituni kuishi miaka 7 akila nyasi kama mnyama.
Ninachosema ni kwamba Mungu hufurahishwa na wanyenyekevu mbele zake,UNYENYEKEVU hubeba mengi ndani mwake,ndio maana unaona Yohana Mbatizaji anamtangulia Yesu Kristo kuhubiri,na ujumbe wake mkuu ukiwa,"tubuni kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia"Yesu Kristo naye anamfuata na ujumbe huo huo,mara baada ya kubatizwa kwake na pia alipomaliza majaribu yale ya Ibilisi,
Tusome,
Haya hapa ni maneno yake Yohana Mbatizaji,
MATHAYO 3:1-2.
Siku zile aliondokea Yohana Mbatizaji akihubiri katika nyika ya Uyahudi,na Kusema,Tubuni;kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.
Haya hapa ni maneno yake Yesu Kristo Mwana wa Mungu,akiyarudia yale yale ya Yohana Mbatizaji,
MATHAYO 4:17.
Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri,na kusema,Tubuni;kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.
Tumeona jumbe zao zikiwa na ujumbe wa kuwa bila toba,bila unyenyekevu ambao ndio unanyoosha mapito yetu hatuwezi kuuona ufalme wa mbinguni,maana yake kama umekaribia,unakaribia ili tuingie ndani mwake,tunaingiaje?tunaingia kuanzia hapa duniani,kivipi?kwa kutubu,kuwa leo naacha dhambi zangu zote unakiri wewe ni mkosaji,kimawazo,kimaneno na kimatendo,hapo lazima pia uombe toba kwa ajili ya vizazi vilivyopita,hapa namaanisha siku ile ya kwanza unapofanywa upya ndani ya Yesu Kristo maana yake unapookoka,unamkiri Yesu Kristo kuwa ni Mwana wa Mungu na ni Yeye pekee aliyekubali,dhihaka,mateso,manyanyaso,dharau,kejeli,pamoja na vingine vyote alivyokutana navyo,alitolewa dhabihu ya ulimwengu ili tupate kupona,tupate kuokolewa,damu yake yenye thamani kupita vyote,ilileta NEEMA sana ulimwenguni na ndio maana kwa sasa Mungu hashushi hasira zake kama ilivyokuwa awali kwenye agano la kale,hata mwanadamu akengeukapo isivyo kawaida ingawa hakuna dhambi isiyo kuwa dhambi mbele za Mungu,damu hiyo ndiyo inayofuta makosa yetu yote tuombapo msamaha kwa kumaanisha,kumaanisha maana yake hurudii tena,ambapo sadaka za kuteketezwa na nyinginezo ikiwemo damu ya upatanisho ya wanyama waliochinjwa na wana wa Israeli haikuweza kumridhisha Mungu Baba kwa asilimia mia,Yesu Kristo alikuja pia kuwahubiria maskini habari njema,maana yake akishaondoka tuwe matajiri Kiroho na Kimwili pia.KUOKOKA maana yake ni kukiri kuwa umekosa,yaani kutubu mbele zake Mungu,kumkabidhi Yesu Kristo mizigo yako yote,kumkubali Yeye kuwa ni Mwana wa Mungu,kuenenda kama amri zake na maagizo yaamrivyo,maana alisema mtu anipendaye ni yule azishikaye amri zangu,kuishi katika utakatifu,kimawazo,kimaneno na kimatendo masaa yote uliyo duniani kuunganishwa na Yesu Kristo,ambapo ndipo utaweza muona Mungu Baba ukisaidiwa na Roho Mtakatifu,na yote tutayapata kwenye NENO LA MUNGU,baada ya KUOKOKA Mungu kupitia Neno lake atakubadilisha utu wa zamani wa ndani na kuhuishwa kuwa kiumbe kipya.
UNYENYEKEVU:Ni jambo linalohitajika kila siku katika maombi yetu,ni suala pekee litakalo tupa haki mbele za Mungu,waweza sema wewe ni mtoaji sana,na unayafuata maagizo yake katika kifungo hicho cha kutoa,lakini nikudhibitishie kuwa wala Mungu hana shida na fedha au dhabihu zozote za kile tumtoleacho maana vyote Duniani ni vyake,aliweka hivyo kwa ajili ya kutafuta daraja la kutuunganisha tusimsahau ili atweze mioyo yetu kuona ilivyo.
Kama huna unyenyekevu yaani kama hukubali makosa yako na kuyawasilisha kabla ya maombi yako hata hayo matoleo ni kazi bure,endapo KIBURI ndicho kitu kisimamacho ndani mwako.
UFALME WA MUNGU HAUPATIKANI KWA KUJIKWEZA(KIBURI AMA JEURI),BALI KWA KUJISHUSHA,AJISHUSHAYE HUKWEZWA,NA AJIKWEZAYE HUSHUSHWA,UKWELI NI KWAMBA HAKUNA TUWEZALO KULITENDA JUU YA MUNGU,ETI KWA AJILI YA VIBURI,JEURI ZETU ZITOKANAZO NA HALI ZETU ZA KIMAISHA.
Ukikutana na kina Mfalme Daudi utaona alizini,pia aliuwa,vivyo hivyo na Musa naye aliua wakiwa utumwani Misri,Mtume Paulo alikuwa muuaji hatari wa Watumishi wa Mungu na mpinzani mkuu wa Injili,ila mwisho wa siku akaja kuwa mtumishi mkubwa,maana alipotambua alitii na kunyenyekea,Samsoni alikubali ushawishi wa Delila,upako wake ukachukuliwa kwa mara ya kwanza kupitia Delila ila alipotambua makosa alikwenda mbele za Mungu akitubu na kuomba upako kwa upya na Mungu alimpa sawia na alivyoomba,Sulemani alikengeuka kwa kuja kuoa wake wa kigeni na kusujudia miungu,jambo ambalo Mungu halipendi,na wengine wengi waliopatwa na madhaifu hayo ya kibinadamu,lakini wote walitumika kwa sababu ya kujitambua na kunyenyekea,kuomba rehema(kukubali umkosaji na waomba msamaha)ndicho kilicho wasaidia wasonge mbele na Mungu kutenda Miujiza mikubwa kupitia wao.
MUNGU NI MWINGI WA REHEMA
YOELI 2:12-13.
Lakini hata sasa,asema BWANA,nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote,na kwa kufunga,na kwa kulia,na kwa kuomboleza;rarueni mioyo yenu,wala si mavazi yenu,mkamrudie BWANA,Mungu wenu;kwa maana yeye ndiye mwenye neema,amejaa huruma;si mwepesi wa hasira,ni mwingi wa rehema,naye hughairi mabaya.
ISAYA 44:22.
Nimeyafuta makosa yako kama wingu zito,na dhambi zako kama wingu;unirudie;maana nimekukomboa.
WAEBRANIA 8:12.
Kwa sababu nitawasamehe maovu yao,
Na dhambi zao,sitazikumbuka tena.
YEYE HUPENDA WANYOFU WA MOYO,NA HUSAMEHE KOSA LOLOTE KWA WANYENYEKEVU,SADAKA ZA WAOVU HATA HAZIKUBALI,HUTAKA REHEMA KWANZA SIO SADAKA,
Tusome mstari huu juu ya Rehema kwanza kabla ya sadaka,Yesu Kristo anasema mwenyewe,maana ya mstari huu ni kwamba ukitoa sadaka bila kuomba toba kwanza wafanya kazi bure,maana sadaka zako hukubalika pale palipokuwa na maombi kwanza ya kuomba rehema(Unyenyekevu) kukubali makosa na kuomba msamaha.
MATHAYO 9:13.
Lakini nendeni,mkajifunze maana ya maneno haya,Nataka rehema,wala si sadaka;kwa maana sikuja kuwaita wenye haki,bali wenye dhambi.
Hapa yatufunza kuwa sadaka za kiburi,jeuri na kujihesabia haki pasipo kunyenyekea kwanza ,kuomba toba ili upate kibali machoni pake si kitu,maana Yeye ataka tujikubali kuwa tumetenda dhambi na kupungukiwa wa utukufu wake WARUMI 3:23,tumehesabiwa haki bure kwa Imani kupitia kufa kwake msalabani.
UNYENYEKEVU NI JAMBO LA AWALI UWAPO KWENYE MAOMBI,KUOMBA REHEMA KWANZA,KUTUMIA JINA LA YESU KRISTO NA KUPITIA DAMU YAKE ITUPATANISHE NA MUNGU BABA,PASIPO HILO UFALME WA MBINGUNI HATUTAUONA.
Tusome na mistari hii kwenye kitabu lengwa cha leo.
ZABURI 51:1-4.
Ee Mungu,unirehemu,
Sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu,
Maana nimejua mimi makosa yangu
Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako,
Na kufanya maovu mbele za macho yako.
Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo,
Na kuwa safi utoapo hukumu.
Tumemuona Mfalme Daudi naye hapo akiomba Rehema na kukubali makosa yake,
UNYENYEKEVU NI NGUZO KUU YA KUKUINGIZA KATIKA UFALME WA MUNGU,KILA ITWAPO LEO UOMBAPO MAOMBI YA AINA YOYOTE ANZA NA HILO.
Namshukuru Mungu,kwa ujumbe huu kupitia Roho Mtakatifu.
UBARIKIWE SANA UUSOMAPO UJUMBE HUU,MUNGU NA AKUONEKANIE NA KUKUWEZESHA KUFIKA SALAMA NDANI YA SAFARI YA KUELEKEA MBINGUNI.
Shalom,Shalom(Amani,Amani).
@ Gideon Kiyyian Ole Kiyiapi.
0 comments:
POST A COMMENT