Mamake mzazi ndiye mkufunzi wake, na licha ya kupoteza ajira yake, mchezo wa kulenga shabaha umekuwa tegemeo la Shehzana Anwar, Mkenya mwenye umri wa miaka 26.
Ndoto ya Shehzana, kushiriki Rio, ilitimia mapema mwaka huu na hivyo basi kumwezesha kuwa Mkenya pekee atakayepiga foleni kulenga shabaha kwenye mchezo wa Olimpiki.
"Nilianza mchezo huu kama mapendelei, lakini baadaye kipaji changu kiligundulika nilipoanza kuibuka mshindi katika mashindano tofauti,'' Alieleza.
Shehzana maarufu 'Kuki', alifuzu kushiriki kwenye Olimpiki baada ya kupata pointi 601 ambayo ni alama iliyohitajika kufuzu. Aidha, hali hii imemfanya Shehzana, kuandikisha alama 610 iliyo sawa na rekodi ya mchezo huo nchini Kenya.
Kulingana naye, licha ya mchezo huo kutokuwa na umaarufu nchini Kenya, amekuwa akijitahidi kwa muda mrefu kuiwakilisha Kenya kwenye Olimpiki.
''Mchezo huu haufahamiki sana Kenya na hautiliwi mkazo kama michezo mingine, lakini nia yangu ni kuiweka Kenya kwenye ramani ya kimatiafa ya mchezo huo,'' anasema.
Shehzana, ambaye pia ni mtoto wa bingwa wa mbio ya magari ya langalanga nchini Kenya, Azar Anwar, atakuwa akiwania medali baada ya kuwa Mkenya wa kwanza wa kujikatia tiketi ya Olimpiki kwa njia ya kufikisha alama zilizohitajika.
Binti huyo ambaye ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto wanne, alianza kushiriki mchezo huo akiwa na umri wa miaka 13.
Kupoteza kazi
Shehzana ambaye alisomea kozi ya saikolojia, alipoteza kazi yake baada ya kuhitajika pakubwa kufanya mazoezi zaidi ili kufuzu kwa Olimpiki.
''Nilipoteza kazi yangu hapa Nairobi kwa sababu ilikuwa vigumu kuendesha kazi na maandalizi ya mchezo wa kulenga Shabaha.
Mbali na wanariadha, waogeleaji, wawakilishi wa raga na kurusha mkuki, Shehzana atakuwa mmoja wa wanamichezo wa Kenya wanaoshiriki Olimpiki ambao wanabeba matumaini ya wakenya ya kuzoa medali Rio.
''Malengo yangu ni kuiwakilisha Kenya vyema na sina wasiwasi kuhusu wapinzani wangu, nitafanya vyema,'' alimaliza.
Shehzana atakuwa uwanjani tarehe 6 Agosti kwenye mashindano ya mchezo wa Kulenga Shabaha.
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT