Rais wa Marekani Barack Obama ameandika makala na kufafanua ni kwa nini yeye hujichukulia kama mtetezi wa usawa na haki za wanawake, ambapo anasema pia kwamba ni jukumu la wanaume kukabiliana na unyanyapaa dhidi ya wanawake.
Kwenye makala hiyo, Rais Obama anasema watu muhimu sana maishani mwake wamekuwa wanawake, na pia anataja kujitolea kwa mke wake, Michelle.
Anahitimisha kwa kusema utetezi wa usawa na haki za wanawake katika karne ya 21 ni "dhana kwamba kila mtu ni sawa, sote tuna uhuru zaidi hivyo."
Makala kamili imechapishwa katika jarida la Glamour.
Mapema mwaka huu, Rais Obama aliambia kongamano kuhusu wanawake mjini Washington kwamba "hivi ndivyo utetezi wa usawa na haki za wanawake ulivyo".
Amesema hayo katika mwaka ambao Bi Hillary Clinton amejipatia nafasi ya kuwa mgombea urais wa chama cha Democratic nchini Marekani, mara ya kwanza kwa mwanamke kuwa mgombea urais wa chama kikubwa nchini Marekani.
Kwenye makala hiyo, Bw Obama anasema manufaa ambayo hakuyatarajia kutoka kwa kazi yake kama rais wa Marekani ni kwamba kuishi ikulu ya White House kulimpa fursa zaidi ya kuwatazama mabinti zake wakikua.
"Jambo moja linalonipa matumaini kuwahusu ni kwamba huu ni wakati mwema sana kwa mtu kuwa mwanamke," anasema Rais Obama.
"Hatua ambazo tumepiga katika miaka 100 iliyopita, miaka 50 hivi, na hata, miaka minane iliyopita, zimechangia sana kuboresha maisha kwa mabinti zangu kuliko ilivyokuwa kwa bibi yangu. Na nasema hilo si tu kama rais lakini pia kama mtetezi wa usawa na haki za wanawake."
Lakini anaongeza kwamba hatua zaidi zinafaa kuchukuliwa kufanikisha usawa, akisema mara nyingi jamii imekuwa ikifungwa na dhana potovu kuhusu wanaume na wanawake na tabia ambazo wanatarajiwa kuwa nazo.
Na anakiri kwamba mzigo wa kuwalea watoto wake umekuwa mkubwa kidogo kwa mkewe.
Bw Obama ameshutumiwa mara kwa mara awali kutokana na matamshi yake kuhusu wanawake, na mwaka 2013 aliomba radhi baada ya kumueleza mkuu wa mashtaka wa California Kamala Harris kama afisa "mrembo zaidi" katika fani yake nchini humo.
bbc.
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT