Mtaalamu wa Teknolojia ya mtambo unaotoa chumvi na baadhi ya madini yasiyotakiwa kwenye maji Ronny Graul kutoka Kampuni ya TRUNZ ya Uswisi akikinga maji yaliyokwisha chujwa kutoka katika moja ya mitambo ya kisasa inayotumika kusafishia maji, wanaomtazama ni baadhi ya wataalamu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji waliohudhuria mafunzo ya matumizi ya mtambo huo yaliyofanyika Juni 6,2016 Jijini Dar es Salaam.
Mtaalamu wa Teknolojia ya mtambo unaotoa chumvi na baadhi ya madini yasiyotakiwa kwenye maji Ronny Graul kutoka Kampuni ya TRUNZ ya Uswisi akionyesha jinsi mtambo huo unavyofanya kazi, wanaomtazama ni baadhi ya wataalamu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji waliohudhuria mafunzo ya matumizi ya mtambo huo yaliyofanyika Juni 6,2016 Jijini Dar es Salaam.
Na Jacquiline Mrisho- MAELEZO
Wizara ya Maji na Umwagiliaji imepewa mafunzo na Kampuni ya TRUNZ kutoka Uswisi juu ya mitambo inayosafisha maji yenye chumvi na madini yasiyotakiwa katika maji ili kusaidia ongezeko la upatikanaji wa maji safi na salama nchini.
Mafunzo hayo yametolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mtaalamu wa Teknolojia kutoka katika Kampuni hiyo, Ronny Graul ambaye ameelezea na kuonyesha jinsi mitambo hiyo inavyosafisha maji yenye chumvi au madini yasiyotakiwa hadi kuwa safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
“Mitambo hii inatumia nguvu ya jua na umeme kidogo sana lakini inafanya kazi kubwa ya kusafisha maji yenye chumvi na madini ambayo hayahitajiki katika maji yakiwemo madini ya floride, chuma,zinki, shaba pamoja na naitreti na kuyaacha maji yakiwa safi na salama katika viwango vinavyohitajika na Shirika la Afya Duniani (WHO)”,alisema Graul.
Mtaalamu huyo ameongeza kuwa mitambo hiyo inapatikana kiurahisi na ina uwezo mkubwa wa kusafisha maji hasa kwa maeneo yenye visima vya maji yenye chumvi pamoja na madini yasiyotakiwa ambapo kwa Tanzania maeneo yaliyokithiri kwa kuwa na maji yenye chumvi nyingi ni Mtwara,Singida, Dar es Salaam na Pwani.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Maji Mjini wa wizara hiyo, Muhandisi Mary Mbowe alisema kuwa lengo la Wizara kuomba mafunzo hayo ni kufahamu namna gani mitambo hiyo inavyofanya kazi ili kama itakidhi vigezo iweze kununuliwa na kupelekwa katika maeneo sugu yenye maji ya chumvi hivyo, kusaidia Watanzania wengi kupata maji safi na salama.
Kwa upande wa Mkurugenzi Msaidizi wa Ubora wa Maji Philip Chacha pamoja na wataalamu wengine wa ubora wa maji kutoka wizarani hapo wamesema kuwa wamejidhihirisha kwa ubora wa mitambo hiyo na jinsi ilivyo na uwezo mkubwa wa kusafisha maji kwa kwa muda mfupi hivyo, itaweza kuokoa maisha ya Watanzania hasa waishio vijijini kwani wataepuka magonjwa yanayosababishwa na maji yasiyo safi na salama.
Mitambo hiyo imeundwa na mitambo miwili inayofanya kazi kwa pamoja ambapo mtambo wa kwanza unajulikana kwa jina la AQUIFIER 200 unaotumika kuondoa chumvi na madini yasiyotakiwa katika maji na mtambo wa pili unaitwa SURVIVOR 300 ambao unachuja maji na kuyaacha yakiwa safi na salama kwa kunywa bila kuchemsha wala kutia dawa ya kusafishia.
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT