Mgombea urais wa chama cha Democratic nchini Marekani Hillay Clinton, amemlaumu mshindani wake wa chama cha Republican Donald Trump kwa kuyaweka mbele maslahi yake kuliko sheria na sera za taifa la Marekani.
Inafuatia ripoti katika jarida la Newsweek inayodai kuwa kampuni inayomilikiwa na Donald Trump ilikiuwa vikwazo vya kibiashara vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba miaka ya tisini.
Jarida hilo linadai kuwa maafisa wakuu wa kampuni hiyo walipeleka dola 68,000 nchini Cuba, wakati matumizi yoyote bila ya idhini ya serikali yalikuwa ni kinyume na sheria.
Meneja wa kampeni ya Bwana Trump anasema kuwa alielewa kuwa pesa zililipwa lakini Trump aliamua kutowekeza huko.
Sasa kamati inayoendesha kampeni ya Trump imetakiwa kujibu maswali yanayotokana na tuhuma hizo.
Mapema wiki hii Trump alikuwa kwenye mitaa ya mji wa Miami yenye watu wa asili ya Cuba, ambapo alipata kikombe cha kahawa kwenye mkahawa mmoja maarugu jinsi walivyofanya watanguliza wake.
Hata hivyo jitihada zake huenda zikaathiriwa na vitendo vya siku za nyuma.
bbc.