Mgombea
wa urais nchini Marekani mwenye utajiri mkubwa Donald Trump anajindaa
kukiunganisha chama cha Republican kilichogawika wakati akijiweka tayari
kuchuana na mgombea wa chama cha Democrat Hillary Clinton.
Jumatano
usiku mbunge mwandamizi wa chama cha Repulican katika baraza la seneti
Mitch McConell amemuunga mkono rasmi Trump kama mgombea wa chama hicho
cha Republican ili kuzuwiya muhula wa tatu wa chama cha Democrat cha
Rais Barack Obama anayemaliza muda wake.
McConell
amesema Trump ambaye anachukuliwa ndie atayekuwa mgombea wa urais kwa
tiketi ya chama hicho hivi sasa ana fursa na wajibu wa kukiunganisha
chama chao katika kutimiza malengo yake.
Ushindi
mkubwa wa Trump katika uchaguzi wa mchujo hapo Jumanne katika jimbo la
Indiana umewalazimisha wagombea wengine wa chama hicho kubwaga manyanga
Ted Cruz na baadae John Kasich gavana wa Ohio ambaye amefanya hivyo hapo
jana na kumwachia tajiri huyo bila ya mpizani kuwania tiketi ya
kukiwakilisha chama hicho.
Wafuasi
wa gavana wa Ohio John Kasich wameelezea masikitiko yao na kuvunjika
moyo baada ya kutangaza kwamba anasitisha kampeni yake ya kuwania urais.
Linda
Ayish amesema "Nimevunjika moyo kwamba amesitisha kampeni yake.Nimekuwa
nikimfahamu gavana Kasich kwa takriban miaka 40. Ni mtu kama vile alivyo
katika uhalisia wake. Nafikiri ameendesha kampeni nzuri na nafikiri
mwishowe ujumbe wake haukuitikiwa lakini hiyo ndio siasa."
Umoja katika chama
Trump
mwenye umri wa miaka 69 amekiambia kituo cha televisheni cha Fox News
kwamba sasa watakiunganisha chama na watauwaunganisha watu pamoja.
Lakini
kutokana na kutoungwa mkono kwa kiwango kikubwa sana kuwahi kushuhudiwa
miongoni mwa wagombea wa urais nchini Marekani wa kipindi cha sasa na
wasi wasi ndani ya chama chake chenyewe juu ya tabia yake ya jazba
tajiri huyo mara moja ameanza kuchukuwa hatua ya kuondowa wasi wasi juu
ya namna atakavyoingoza nchi hiyo.
Ameliambia
gazeti la New York Times kwamba anajuwa watu hivi sasa hawana uhakika
Rais Trump atakuwa wa aina gani. Amesema lakini mambo yatakuwa mazuri
kwamba hagombanii urais ili kuiyumbisha nchi.
Kitendawili cha mgombea mwenza
Trump pia
ameanza kutafakari wazo la yule anayeweza kuwa mgombea mwenza wake kwa
kukiambia kituo cha televisheni cha ABC News anataka "mtu mwenye uzoefu
wa kisiasa" ili kuchanganisha na wake wa kibiashara.
Majina
yanayotajwa ni pamoja na seneta Rob Portman wa jimbo la Ohio lenye
wapiga kura wengi wasioamuwa chaguo lao na gavana wa jimbo la South
Carolina Nikki Haley.
Trump
mwenyewe binafsi amesema angeliweza kumfikiria Kasich mbunge wa zamani
ambaye amesaidia kuweka uwiano katika bajeti ya serikali kama mgombea
mwenza wake.
Kivumbi
kikubwa kinachomkabili tajiri huyo kinatoka kwa mgombea wa Demokratik
Hilary Clinton mwenye umri wa miaka 68 ambaye anatarajia kuwa Amiri
Jeshi Mkuu wa kwanza mwanamke nchini Marekani ambapo kwa mujibu wa
uchunguzi wa maoni yuko mbele ya Trump kwa asilimia 54 dhidi ya 41.DW
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT