bongo satellite.: Tanzania-Siasa.
Breaking News
Loading...
Showing posts with label Tanzania-Siasa.. Show all posts
Showing posts with label Tanzania-Siasa.. Show all posts

Monday, 29 August 2016

Meya wa Ukawa aungana na Rais John Magufuli.

Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kwiyeko

Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kwiyeko akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo. Picha na Salim Shao .
Dar es Salaam. Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko (Chadema), ameungana mkono na Rais John Magufuli, kuwakingia kifua wafanyabiashara wadogo maarufu Wamachinga akitaka wasibughudhiwe na mtu yeyote.
Akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari, Kuyeko alisema wafanyabiashara hao waendelee kufanya shughuli zao katikati ya jiji.
“Machinga waendelee kufanya kazi bila bugudha. Kusiwe na mtu yeyote wa kuwasumbua,” alisema.
Kauli hiyo ya Kuyeko inaweka mkazo kwenye kauli aliyoitoa Rais Magufuli hivi karibuni alipokuwa ziarani jijini Mwanza alipotengua mpango wa kuwaondoa Machinga katikati ya Jiji la Mwanza uliokuwa umepangwa kutekelezwa Agosti.
Badala yake, Rais Magufuli aliwataka viongozi wa jiji hilo kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa na mbunge wa Nyamagana, kushirikiana kuandaa maeneo ya kuwapeleka Wamachinga hao badala ya kuwaondoa huku kukiwa hakuna maeneo mbadala yaliyotengwa kwa ajili ya wao kufanyia biashara.
Meya huyo alisisitiza kuwa Rais Magufuli ni Rais wa Watanzania wote, haijalishi kauli hiyo aliitolea sehemu gani, bali inatosha kutambua tu kuwa aliwasemea wamachinga wote wakiwamo wa Jiji la Dar es Salaam. “…Waendelee kukaa mjini kufanya biashara hadi baraza la madiwani litakapo kaa (tarehe itapangwa) na kuamua maeneo watakayopangiwa kwa ajili ya wao kufanyia biashara. Kutoa kauli za kuwataka leo waondoke na kurudi ni kuwachanganya.”
“Wamsikilize nani wamuache nani. Rais Magufuli ameshasema waendelee kufanya biashara katikati ya jiji hadi mpango wa kuwapatia maeneo yao utakapokamilika,” alisema.
Msisitizo wa kauli ya meya huyo ya kuwakingia kifua Machinga, unalenga kuwaondoa hofu wafanyabiashara hao ambao walianza kuingiwa na wasiwasi baada ya Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwaondoa katika maeneo ya Soko la Kariakoo na barabarani, hususan karibu na barabara za mabasi ya mwendo kasi.
Kupitia agizo hilo alilolitoa hivi karibuni, Simbachawene alisema kurejea kwa wafanyabiashara katika maeneo hayo kumeleta usumbufu na uchafu wa mazingira katika maeneo mengi ya jiji, hivyo Makonda asilegeze kamba katika suala hilo.
Mwananchi.

Ole Sendeka amsifu Lowassa.

Rais John Magufuli akisalimiana na Waziri Mkuu

Rais John Magufuli akisalimiana na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa walipohudhuria Misa ya Jubilei ya Dhahabu ya Ndoa ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa katika Kanisa la Mtakatifu Petro jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Ikulu 
Dar es Salaam. Msemaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka amesema Edward Lowassa ni muungwana na kwamba asingeweza kuacha kumsalimia kwa kumpa mkono Rais John Magufuli.
Ole Sendeka amesema jana: “Namfahamu Lowassa ni muungwana hawezi kuacha kusalimiana kwa kupeana mkono na Rais. Wamekutana viongozi, Rais na waziri mkuu mstaafu hawawezi kuacha kusalimiana.”
Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema aliyechuana na Rais Magufuli katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 mwaka jana, juzi walikutana kwa mara ya kwanza na mpinzani wake huyo tangu kinyang’anyiro hicho kilipomalizika.
Viongozi hao walikutana kwenye misa ya jubilei ya dhahabu ya ndoa ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa na mkewe Anna katika Kanisa la Mtakatifu Petro.
Mwananchi.

Kuikosoa Serikali siyo uhaini-Lissu.



Mwanasheria wa Mkuu Chadema, Tundu Lissu

Mwanasheria wa Mkuu Chadema, Tundu Lissu 
By Joster Mwangulumbi, Mwananchi; jmwangulumbi@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Mwanasheria wa Mkuu Chadema, Tundu Lissu amesema Katiba ya mwaka 1965 ilifuta vyama vingi ikabaki Tanu hali iliyoondoa uwezekano kikatiba wa kupinga au kukosoa utawala wa Awamu ya Kwanza bila kukabiliwa na nguvu za dola na kushtakiwa.
Lakini marekebisho ya mwaka 1992 yaliyotokana na Waraka Na 1 wa Serikali, yalirejesha mfumo wa vyama vingi ambamo ndani kuna uhuru na haki kisheria na kikatiba kuipinga na kuikosoa Serikali.
Mwanasheria huyo amesema kwa kuzingatia Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992, kuipinga na kuikosoa Serikali si uhaini wala kosa kwani vyama vya upinzani vimepata uhalali huo kisheria na ndiyo maana vinasema haviwezi kuona Serikali ya Rais John Magufuli ikitumia mamlaka isiyokuwa nayo kwa kusigina Katiba na sheria.
Amesema tofauti kubwa kati ya utawala wa Mwalimu Nyerere na Rais Magufuli ni mamlaka waliyonayo kikatiba.
Mwananchi. 

Lema hoi kwa kutokula.



Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema 
By Zulfa Musa, Mwananchi ; zmusa@mwananchi.co.tz
Arusha. Hali ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema aliyeko mahabusu jijini hapa tangu alipokamatwa na polisi Ijumaa iliyopita, inadaiwa kuwa ni mbaya baada ya kugoma kula akishinikiza kupelekwa mahakamani.
Mwanasheria wa mbunge huyo, John Malya amesema hali ya mbunge huyo si nzuri, huku akisisitiza kuwa kama asipopelekwa mahakamani mpaka kufikia leo saa tano asubuhi, wataandika barua Mahakama Kuu, ili itoe agizo kwa polisi kumpeleka mahakamani.
Tangu mbunge huyo alipokamatwa akiwa nyumbani kwake, amegoma kula huku akishinikiza kupelekwa mahakamani.
Awali, Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alimkariri mbunge huyo akisema yuko tayari kufa kwa kutokula kama ataendelea kuwekwa mahabusu.

Profesa Lipumba,Magdalena Sakaya na Abdul Kambaya Wavuliwa Uanachama CUF.


Chama Cha Wananchi (CUF) kimewasimamisha uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Bara, Magdalena Sakaya.
Uamuzi huo umetolewa jana na Baraza Kuu la Chama hicho lililofanya mkutano wake visiwani Zanzibar kwa lengo la kuwajadili wanachama kadhaa wakiwemo vigogo hao. Sakaya amevuliwa nyadhifa zote ndani ya chama kabla ya kusimamishwa.
Taarifa kutoka ndani ya Mkutano huo zimeeleza kuwa Baraza hilo limewaadhibu wanachama 15 wakiwemo Sakaya ambaye pia ni mbunge wa Kaliua.
Mbali na vigogo hao, wengine waliopigwa rungu na Baraza Kuu la CUF ni pamoja na Katibu wa Baraza la Wazee, Shashi Lugeye, Thomas Malima na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano, Abdul Kambaya.
Aidha, Baraza hilo limemsimamisha uanachama Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma. Hatua hii inaweka matatani ubunge wa Sakaya na Nachuma kwani wakifikia hatua ya kufukuzwa watakosa sifa za kuendelea kuwa wabunge.
Lipumba na Sakaya hawakupata nafasi ya kujitetea kutokana na kutohudhuria mkutano huo wakati Shashi alipata nafasi ya kujitetea kutokana na uwepo wake lakini utetezi wake haukuzaa matunda. Katiba ya chama hicho haiwapi nafasi wabunge hao kukata rufaa kutokana na uamuzi wa Baraza hilo.
Uamuzi huo umekuja ikiwa ni siku chache baada ya Mkutano Mkuu Maalum wa Chama hicho uliolenga kumchagua Mwenyekiti Mpya kuvunjika kutokana na kuwepo vurugu kubwa baada ya Profesa Lipumba kuingia ndani ya ukumbi huo na wafuasi wake wakitaka barua yake ya kutaka kurejea kwenye nafasi yake ijadiliwe na kukubaliwa.
Hata hivyo, kura zilizopigwa na wajumbe wote zaidi ya 800, ni kura 14 pekee zilizotaka Profesa Lipumba aendelee na nafasi ya uenyekiti.