VISASI VYASHEHENI MGOGORO WA WAKULIMA NA WAFUGAJI KIMANGE. | bongo satellite.
Breaking News
Loading...

Tuesday, 6 September 2016

VISASI VYASHEHENI MGOGORO WA WAKULIMA NA WAFUGAJI KIMANGE.

n1Shamba la Bakari Ally kijiji cha Kimange wilayani Bagamoyo,anaedai shamba lake limeliwa mazao na ng’ombe wa wafugaji jamii ya wamang’ati ambalo linaonekana lina mabua yaliyovunwa mahindi na sio mazao kama anavyodai na kusababisha mgogoro . (Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
WATU wawili jamii ya waman’gati wanashikiliwa na polisi,kwa kosa la kumnyang’anya gobore mkulima aliyejulikana kwa jina la Bakari Ally,kufuatia vurugu zilizotokea baina ya wakulima na wafugaji huko kijiji cha Kimange wilayani Bagamoyo.
Imedaiwa chanzo cha mgogoro huo ni ng’ombe walioingia katika shamba la mkulima huyo, Ally ambapo aliamua kuwaua baadhi ya ng’ombe walioingia shambani kwake kwa kuwapiga risasi kwa kutumia gobore hilo.
Aidha kufuatia sakata hilo mwanamke mmoja wa jamii ya kifugaji anadaiwa kudhalilishwa kwa kuingiliwa kinguvu kimapenzi na baadhi ya watu wasiojulikana.
Kiongozi wa wafugaji katika kijiji cha Kimange ,Deogratias Mereqwa alisema, tukio hilo limetokea juzi baada ya ng’ombe kumtoroka kijana aliyekuwa akichunga na kisha kuingia katika shamba la Ally ambalo lilikuwa na mabua ya mahindi.
Alisema shamba hilo sio kama lilikuwa na mazao bali ni mabua ambayo yalishavunwa mahindi ambapo mzee huyo alipoona ng’ombe wameingia shambani kwake alichukua uamuzi wa kuwapiga risasi za gobore lake.
“Alipiga risasi kwa kutumia gobore lake mwenyewe na kisha kupiga kelele ambapo kundi kubwa la wakulima wenzake lilifika na kwenda kwa mwenye ng’ombe ambako waliiba fedha na kumfanyia vitendo vibaya mama mwenye ng’ombe”alisema Mereqwa.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa wafugaji anasema mwanamke aliyeingiliwa kimapenzi alifanyiwa vitendo hivyo kwa zamu na watu wasiojulikana na amelazwa katika hopitali ya wilaya ya Bagamoyo.
Mereqwa alidai kwamba idadi kamili ya mifugo iliyouwawa haijajulika kutokana na ng’ombe wote waliokuwa katika shamba hilo wametawanyika na hawajarudi nyumbani.
Mkazi wa Kimange ,Halima Twaha ,alisema migogoro ya wakulima na wafugaji sasa imekua .
Nae mkulima katika eneo hilo,George Kitilya ,anahofia ipo siku italeta madhara zaidi ya hayo yaliyotokea kwani kila upande unahisi unaonewa pale mgogoro wao unapofikishwa katika ofisi za serikali ya kijiji,kata ama ngazi za juu.
Aliiomba serikali kuanglia suala hilo kwa kina na kulifanyia suluhisho ili kuondoa visasi vinavyoendelea na madhara ambayo yanaweza kujitokeza.
Kitilya alisema imefikia hatua ya wamang’ati hao kwenda kuwafanyia fujo wakulima majumbani mwao nyakati za usiku huku wakiwa na mikuki.
Alisema wanaogopa na wengine kuamua kukimbia miji ya kwa kuhofia kudhuriwa na wafugaji kutokana na hasira na chuki walizojiwekea.
Hata hivyo alisema katika shamba lake ngo’ombe waliwahi kula ufuta aliopanda na kupata hasara.
Kwa upande wake, mganga mfawidhi wa hopitali ya wilaya ya wilaya ya Bagamoyo, dk. Tumaini Bairon,alikiri kupokewa kwa mwanamke huyo ambae baada ya kufanyiwa vipimo imebainika kweli amefanyiwa vitendo hivyo na anaendelea kupatiwa matibabu.
Kamanda wa polisi mkoani Pwani,kamanda Boniventure Mushongi,alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema wanaendelea na uchunguzi .
Kamanda Mushongi alieleza ,kwasasa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo anaendelea kwa hatua zaidi ili kurejesha makubaliano kati ya makundi hayo na atawapelekea taarifa ya hatua aliyofikisha na ndipo yeye atakuwa na majibu zaidi.
Migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani Bagamoyo inaonekana kukithiri hali inayowaumiza vichwa viongozi mbalimbali na polisi kutokana na pande hizo kwenye maeneo mengine kushindwa kuheshimiana na kila upande ukijiona zaidi ya mwenzake.
Ndani ya mwezi mmoja ni matukio matatu makubwa yatokanayo na migogoro hiyo yametokea kwa nyakati tofauti wilayani humo ambapo hivi karibuni huko Kitomondo,kata ya Makurunge ,mfugaji aliuwawa na mkulima alijeruhiwa.
Kufuatia hali hiyo mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo,aliamua kuunda kamati ya uchunguzi kwa ajili ya kuchunguza kifo hicho na tatizo kubwa linalosababisha kukua kwa migogoro hiyo. (P.T)
Mjengwa Blog.
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT