Umoja wa Mataifa umekubaliana kuongeza jitihada za kumaliza janga la UKIMWI, ifikapo mwaka 2030, ingawa Urusi imetaka kutowalenga zaidi watumiaji wa dawa za kulevya na wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Makubaliano hayo ya kisiasa yamefikiwa na wanachama 193 katika mkutano mkuu, ulioweka msisitizo juu ya mahitaji ya kuwasaidia wanaotumia dawa za kulevya kwa kujidunga sindano, wanaojihusisha na biashara ya ngono, wanaobadilisha jinsia na wafungwa ambao wapo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virus UKIMWI.
Maambukizo ya Virusi vya UKIMWI yamekuwa yakipungua katika muongo mmoja uliopita, lakini bado kuna kiasi ya watu Milioni 36.7 duniani kote wanaoishi na Virusi vya UKIMWI ama UKIMWI, na wengi wao wakiwa katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia UKIMWI, UNAIDS, Michel Sidibe amesema ndiko kuna idadi kubwa ya watu wanaotumia dawa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amewaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba UKIMWI bado ni tishio, kwa hiyo mataifa bado yana nafasi ya kuhakikisha yanabadilisha hali ya janga hilo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Ban ametaka kutolewa kwa huduma na dawa kwa watu wote wanaoishi na Virusi vya UKIMWI bila ya ubaguzi. Aliwalenga zaidi vijana wadogo, wahamiaji, wanawake na wasichana, wanaofanya biashara ya ngono, wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, wanaojidunga dawa za kulevya, wanaobadilisha maumbile na wafungwa.
Makubaliano haya yanatokana na mipango ya awali ya Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI yaliyopitishwa miaka mitano iliyopita, kwa kuweka msisitizo zaidi kwa kwale walioko kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi. Makubaliano hayo yamelenga maeneo matatu yanayootakiwa kufikiwa ifikapo mwaka 2020, ambayo ni kupunguza maambukizi mapya ya Virus vya UKIMWI, kupunguza idadi ya vifo na kuondoa unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI.
Urusi ilitaka mabadiliko ya mkakati huo mpya kuangazia sheria za kitaifa na namna zinavyoyataja makundi ya wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, watumiaji wa dawa za kulevya na wafungwa. Walisema wanadiplomasia na makundi ya kiraia, Jumanne hii.
Mabadiliko hayo yalipingwa vikali kutokana na hofu kwamba yataruhusu Urusi, Iran na nchi nyingine zinazochukulia mapenzi ya jinsia moja kama uhalifu kuzuia dawa za kupunguza makali ya UKIMWI na huduma nyingine kwa wanaume hao.
Mkutano huo wa siku tatu, ulianza kwa ombi la mjukuu wa aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Indaba ambaye baba yake alikufa kwa UKIMWI mwaka 2005, akiwataka viongozi wa nchi 35 zinazozuia watu walioathirika kuingia nchini mwao, ikiwa ni pamoja na Urusi na Singapore kuondoa marufuku hiyo.DW
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT