Watu zaidi ya 60,000 wametakiwa kuondoka upesi kutoka kwenye mji wa Fort McMurray, Canada kutokana na moto mkubwa ambao unaendelea kuenea.
Moto huo kutoka porini umeathiri sana maeneo makubwa ya mkoa wa Alberta.
Nyumba kadha zimeteketezwa na majivu yamekuwa yakianguka katika mji huo wa Fort McMurray.
Wakazi wanaotoroka wamesababisha msongamano mkubwa katika barabara kuu inayotoka mji huo unaopatikana kilomita 380 kaskazini mwa Edmonton.
Shughuli hiyo ya kuwaondoa wakazi kutoka kwa mji wa Fort McMurray, unaopatikana eneo lenye mchanga wenye mafuta, ndiyo kubwa zaidi katika historia ya Alberta.
"Ukitoka tu nje, majivu yanakuangukia. Unaona majivu yakielea angani,” mkazi mmoja aliyetambuliwa kama Mark Durocher amenukuliwa na gazeti la Globe and Mail.
Nyumba katika mitaa miwili zimeteketezwa kabisa na moto huo sasa umesambaa na kufikia barabara ya Highway 63 inayoelekea mji wa Fort McMurray kutoka kusini.
Wazimamoto wanaendelea kukabiliana na moto huo lakini maafisa wameomba usaidizi zaidi.
Helikopta inatumiwa kujaribu kudhibiti moto huo.
Kufikia sasa hakujaripotiwa taarifa zozote za majeruhi.
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT