SARATANI ni chembechembe zisizokuwa za kawaida zinazozaliana kwa haraka kwenye mwili wa binadamu bila mpangilio maalumu.
Tafiti zinaonesha kwamba hakuna sababu maalumu inayojulikana kusababisha saratani, ila kuna vichocheo vinavyoweza kusababisha saratani. Vichocheo hivyo viko katika makundi mbalimbali kama vile matumizi ya kemikali, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, utumiaji wa vyakula vyenye mafuta kupita kiasi, unene kupita kiasi pia kutofanya mazoezi kwa watu wanene.
Ni ukweli usiopingika kuwa saratani imekuwa chanzo cha magonjwa na vifo. Inakadiriwa kuwa takribani wagonjwa wapya 45,000 hugundulika kila mwaka wakiwa na saratani za aina mbalimbali kutokana na kuchelewa kugundulika mapema. Aidha, ugonjwa wa saratani umekuwa tishio katika nchi za Afrika zilizo chini ya Jangwa la Sahara. Hapa nchini, tafiti za kitaalamu kuhusu afya ya binadamu zinaonesha miongoni mwa magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo na upotevu wa nguvu kazi.
Zipo saratani za aina mbalimbali. Nazo ni saratani ya shingo ya kizazi, matiti, utumbo mpana na saratani ya tezi dume. Katika mkutano wa 10 wa kufanya mapitio juu ya hatua zilizochukuliwa na nchi za Afrika kukabiliana na saratani, jijini Addis Ababa Ethiopia, inaelezwa hali halisi ya maradhi haya. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alihudhuria mkutano huo, takribani wagonjwa wapya 45,000 wa saratani wanagundulika kila mwaka.
Kati yao, asilimia 38 ni wa saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake, asilimia 14 saratani ya ngozi, asilimia 10 saratani ya matiti na asilimia nne ni ya tezi dume. Aidha, takribani watu 35,000 hufariki kila mwaka kutokana na saratani. Ummy anaeleza kuwa kutokana na ukubwa wa tatizo, serikali imepitisha sera za kitaifa na miongozo mbalimbali ya kukabili maradhi haya. Aidha, inatoa elimu kwa jamii na watoa huduma za afya .
Serikali imeanzisha huduma za upimaji wa saratani katika hospitali na vituo vya afya zaidi ya 300 na huduma za tiba kupitia Hospitali ya Saratani ya Ocean Road. Waziri anasema serikali inaendelea kupanua wigo wa matibabu ya saratani katika Hospitali ya Bugando Mwanza na KCMC – Kilimanjaro. Anasema serikali itaanza kutoa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa watoto wenye umri wa miaka kati ya tisa na 13 kukabiliana na changamoto ya maradhi hayo nchini. Saratani ya shingo ya kizazi inaambukizwa na virusi vinavyojulikana kama Human Papiloma Virus (HPV).
“Tumeamua kuteua kundi la watoto wa rika dogo kwani wengi wao katika umri huo wanakuwa bado hawajaanza kujihusisha na vitendo vya mapenzi,” anasema Waziri Ummy. Katika bajeti ya mwaka 2016/17 Serikali imepanga kuipatia Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kiasi cha Sh bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa dawa ikilinganishwa na Sh milioni 600 zilizokuwa zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2015/16.
Mtafiti na bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya saratani, kutoka Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam, Dk Walter Kweka anaeleza saratani kuwa miongoni mwa majanga yanayonyemelea kila Mtanzania. Anataja ongezeko la ugonjwa huu linachangiwa na sababu za mazingira, vyakula, sababu za kurithi na mtindo wa maisha wa watu wengi mijini na vijijini. Dk Kweka anataja aina kuu za saratani zinazoongoza kuathiri maisha ya watu wengi nchini ni ya shingo ya kizazi, tezi dume, utumbo mpana na saratani ya matiti kwa wanaume na wanawake.
Saratani shingo ya kizazi Dk Kweka anasema miongoni mwa saratani zote, ya kizazi inaongoza kwa kusababisha vifo kwa wanawake. Wapo wanaokumbwa na ugonjwa huu kwa sababu za kurithi ndani ya koo. Wanawake walioanza kufanya ngono katika umri mdogo na wale wenye mpenzi zaidi ya mmoja, pia ni miongoni mwa waathirika wa ugonjwa huu ambao husababishwa na virusi vijulikanavyo kama Human Papiloma Virus (HPV).
Mwanamume ndiye hubeba virusi hivi ambavyo mwanamke huambukizwa kwa njia ya kujamiiana. Miongoni mwa mambo yanayodhihirisha kuwa mtu ana saratani hii, ni maumivu wakati wa kujamiiana, kutokwa na majimaji yenye harufu mbaya au uchafu usio wa kawaida ukeni. Pia kutokwa na damu kidogo au nyingi ukeni wakati wa kujamiiana au kutokwa damu ukeni kwa wanawake waliokoma hedhi.
Dalili nyingine ni maumivu sehemu ya nyonga au chini ya tumbo, kuvimba kwenye kinena, kutokwa na damu kidogo au nyingi ukeni wakati ambao mwanamke hayuko kwenye hedhi. Dk Kweka anasema zaidi ya asilimia 80 ya wanawake wanaougua saratani hiyo hufariki ndani ya miaka mitano kwa kuwa hufika hospitali wakiwa wamechelewa. “Upimaji wa saratani ukifanyika kwa ufasaha, unasaidia kugundua tatizo mapema hivyo mhusika hupata fursa ya kutibiwa mapewa, ni vyema wanawake wakajenga tabia ya kufanya uchunguzi angalau mara moja kwa mwaka,” anasisitiza Dk Kweka.
Tanzania inakadiriwa kuwa zaidi ya wanawake milioni 14 walio katika umri wa kuzaa kuanzia miaka 18 hadi 45 wako kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya shingo ya kizazi. Takwimu za utafiti zinaonesha, wanawake wa Kitanzania wanaopata saratani hii kwa mwaka ni 7,304 na wanaofariki kutokana na saratani hii ni 4,216. Sababu inayochangia vifo ni uwezo mdogo wa kumudu gharama za matibabu, kupuuzia kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali zinapojitokeza dalili za awali.
Wengine hufika hospitalini tatizo likiwa kubwa na baadhi yao hubakia nyumbani wakiamini kuwa wamefanyiwa vitendo vya kishirikina. Saratani hii hujitokeza wakati ikiwa imesambaa na ni vigumu kuitambua mpaka vipimo vya kitaalamu vinapofanyika. Ikigundulika, tiba hufanyika kupitia upasuaji kuondoa seli zote zilizoathirika au kuondoa kizazi kuokoa maisha ya mama. Saratani ya matiti Inaongoza kushambulia wanawake walio katika umri wa kuzaa; miaka 18 hadi miaka 45.
Katika Afrika Mashariki, inakadiriwa wagonjwa wapya wa saratani ya matiti kwa mwaka wanafikia 18,000. Kati yao, 10,000 hufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huo. Dalili za saratani ya matiti ni uvimbe mgumu kwenye titi au kwapani, kupata mabadiliko ya umbo au ukubwa wa titi. Pia kunakuwapo mabadiliko ya rangi ya ngozi ya titi ambayo huonekana na mikunjo kama sehemu ya nje ya ganda la chungwa. Dalili nyingine ni mwanamke kuwa na chuchu zilizoingia ndani na wakati mwingine zinazotoa majimaji machafu au damu.
Mwaka 2008 inakadiriwa kuwa kulikuwa na zaidi ya wagonjwa wapya 2,500 waliogunduliwa kuwa na saratani ya matiti. Kati ya hao, wagonjwa 300 ndiyo walipata tiba katika ya Hospitali ya Ocen Road. Zaidi ya asilimia 90.7 ya wagonjwa wanaofika katika Hospitali ya Ocean Road wanakuwa wamechelewa na ugonjwa unakuwa katika hatua ya juu. Dk Kweka anasisitiza jamii kuchukua hadhari mapema kujikinga na maradhi hayo kuliko tiba.
“Mgonjwa anapochelewa kufika hospitalini na hali yake ikawa mbaya, matibabu yake ni ghali na yanaambatana na uvunaji au uondoaji wa viungo,” anasema. Mathalani, mgonjwa mwenye saratani ya matiti, hufanyiwa upasuaji maalumu kuondoa uvimbe ulioko ndani ya titi na iwapo athari ni kubwa, titi lote huondolewa au huvunwa. Mgonjwa aliyevunwa titi moja huwekwa chini ya uangalizi maalumu wa kitaalamu kwa muda wa miaka mitano akifanyiwa uchunguzi kuangalia kama ana maambukizi kwenye titi la pili.
Anasema zaidi ya watu wapya milioni 10 hufanyiwa uchunguzi kubaini kama wamepata ugonjwa wa saratani kila mwaka duniani. Pia watu milioni sita hupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo na wengine milioni 24.4 kwa mujibu wa takwimu zilizopo wanaishi na saratani.
Wanaume na matiti
Dk Kweka anasema wanaume 1,000 wanaoonwa kwa mwaka katika Hospitali ya TMJ na kufanyiwa uchunguzi wa saratani, asilimia mbili hadi saba hugunduliwa kuwa na saratani ya matiti. Anasema, kwa wanaume hali hiyo hujitokeza katika umri mkubwa kidogo tofauti na akina mama ambao huanza kupata athari kuanzia umri wa miaka 20 mpaka 50. Saratani kwa wanaume hujitokeza kuanzia miaka 45 na kuendelea. Mara nyingi wanaume hupata hali hiyo kutokana na kurithi.
Tezi dume Saratani ya tezi dume ni aina nyingine inayoshambulia wanaume wenye umri kuanzia miaka 50 mpaka 70. Chanzo kikubwa cha saratani hii ni ulaji wa muda mrefu wa vyakula vyenye mafuta mengi, nyama nyekundu, pamoja na sababu za kurithi. Wanaume zaidi ya 1,200 hugundulika kuwa na saratani ya tezi dume kila mwaka. Anasema utafiti wa mwaka 2010 katika Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro ulionesha asilimia 8.9 ya wagonjwa waliofika kufanyiwa uchunguzi wa tatizo la njia ya mkojo waligundulika kuwa na saratani hiyo.
Utafiti kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili unaonesha asilimia 38 ya wanaume wenye tatizo la kukua kwa tezi dume walikutwa na saratani hiyo na walikuwa na umri kati ya miaka 60 na 70. Aidha, wanaume waliokuwa na saratani hii walio na umri chini ya miaka 60 walikuwa asilimia 7.2. Kweka anatoa angalizo akisema, wananchi wengi huchukulia ugonjwa wa saratani kama jambo la kawaida. Anasema wakati mwingine hupuuzia ushauri wanaopewa na wataalamu kuhusu njia sahihi za kujikinga na tiba ya ugonjwa huo.
Anasema hakuna ukoo wa Mtanzania ambao haujawahi kuguswa na tatizo la ugonjwa wa saratani. Anasisitiza juhudi za pamoja zinahitajika kukabili ugonjwa huu. Anahadharisha juu ya matumizi ya sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, matumizi ya kemikali au homoni hasa kwa wanawake wanaolenga kubadili sura na mwonekano wa maumbo ya miili yao. Anasema mambo haya ni miongoni mwa sababu zinachangia kukithiri kwa ugonjwa huu miongoni mwa jamii.
Pia ulaji wa mara kwa mara wa vyakula kama vile chipsi kuku, mayai ya kuku wa kisasa, ulaji wa soseji, baga, matumizi ya kiwango kikubwa cha nyama nyekundu huweka wahusika katika mazingira hatarishi ya kupata ugonjwa huu. “Utafiti nilioufanya kama daktari bingwa mwaka 2013 na kuuchapisha kwenye majarida mbalimbali ya kisayansi, unaonesha kuwa matumizi ya vyakula aina ya chipsi kuku, mayai ya kisasa, soseji ulaji wa baga ni chanzo kikubwa cha watu kupata saratani ya utumbo mpana nchini,” anasisitiza Dk Kweka.
Anasema sababu ya mtu kuwa na umri mkubwa sambamba na ulaji mbaya wa vyakula vyenye kemikali pamoja na tabia kutokwenda hospitalini kupima afya mara kwa mara, imechangia kukuza tatizo miongoni mwa jamii. Mabadiliko ya mtindo wa maisha yameliingiza kundi kubwa la watu kupata saratani. Mtindo wa maisha kuanzia ngazi ya familia umesababisha kila mtu kuwa mwathirika.
Anashutumu watu kuiga umagharibi na kuacha kula vyakula vya asili kama vile ugali wa dona, mboga za majani kama vile matembele, bamia na bilinganya. Asasi isiyo ya kiserikali ya Social Outreach Initiative ( TASOI) ambayo inajishughulisha na utoaji wa elimu na utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii katika masuala ya afya na uchumi, inasisitiza juu ya ulaji.
Katibu Mtendaji wa TASOI, Belinda Mlingo anaeleza kuwa Watanzania walio wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya chanzo, madhara, kinga na tiba sahihi ya saratani. Anasema wakati umefika kwa Watanzania kuamka na kuchukua hadhari dhidi ya ugonjwa huo. Belinda anasisitiza wananchi kuchunguza afya mara kwa mara wakizingatia kwamba, gharama za kutibu saratani ni kubwa na wanaoweza kuzimudu ni wachache.
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT