Lema asomewa mashtaka mawili kortini, amaliza mgomo. | bongo satellite.
Breaking News
Loading...

Tuesday, 30 August 2016

Lema asomewa mashtaka mawili kortini, amaliza mgomo.



Arusha. Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (40) amepandishwa mahakamani kujibu kesi mbili za uchochezi na baadaye kuzua vurugu kubwa mahakamani, polisi walipotaka kumrudisha magereza kutokana na wadhamini wake kuchelewa.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema alikamatwa Ijumaa iliyopita na kwa siku tatu, aligoma kula akilazimisha kufikishwa mahakamani hali iliyomfanya jana kuonekana dhaifu na mnyonge licha ya kumudu kutembea mwenyewe na kuzungumza.
Lema alifikishwa mahakamani jana saa tano asubuhi, akiwa chini ya ulinzi mkali na kushushwa kwenye gari na kupelekwa moja kwa moja katika mahabusu ya mahakamani.
Alipandishwa kizimbani saa 6.12 mchana mbele ya Kaimu Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Desdery Kamugisha kujibu mashtaka ya kusambaza ujumbe kumkashifu Mkuu wa Mkoa Arusha.
Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Serikali, Vincent Njau alisema Lema anatuhumiwa kuwa kwa kutumia simu yake 0764150747 Agosti 20, 2016 alituma ujumbe kwenye namba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo 0766 757575 wenye maneno ya uchochezi.
Njau alitaja maneno hayo kuwa ni “Karibu Tutakudhibiti kama Uarabuni walivyodhibiti Mashoga” ambayo alidai ni ya uchochezi kwa mujibu wa Sheria Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kifungu cha 118(a) na kifungu cha tatu katika sheria iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010. Lema pia alisomewa shtaka katika kesi ya pili namba 252/2016 akituhumiwa kuvunja Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 390 kifungu cha 35 kwa kuhamasisha maandamano yaliyo kinyume cha sheria.
Njau alisema Lema alifanya kosa hilo kati ya Agosti Mosi hadi 26 ambako alisambaza ujumbe kupitia mtandao wa Whatssap wakati akijua ni kosa kisheria.
Njau aliiomba Mahakama isimpe dhamana kwa kuzingatia kifungu namba 148 kifungu kidogo cha 5(d) kwa kuwa zipo taarifa za kiintelejensia ambazo zinalazimu kuomba kuzuia dhamana kutokana na usalama wake.
Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na mawakili wanne wanaomtetea Lema; John Mallya, James Lyatuu, Reygod Nkya na Shaki Mfinanga.
Wakili Mallya alisema hoja ya kumnyima dhamana ni dhaifu na kifungu alichokisema wakili wa Serikali hakizungumzii taarifa za kiintelejensia.
Alisema pia pingamizi hilo halina nguvu kisheria kwani wakili wa Serikali alipaswa kuwasilisha maombi rasmi yenye hati ya kiapo ya kupinga dhamana na zisemwe hizo taarifa za kiintelejensia.
Pia, alieleza kuwa kosa la mtuhumiwa lina dhamana na kuiomba Mahakama kutupa pingamizi la wakili wa Serikali kuzuia dhamana.
Baada ya hoja hiyo, Hakimu Kamugisha alikubaliana na hoja za utetezi kuwa dhamana ni haki ya msingi ya mtuhumiwa hasa kulingana na kosa lake.
Hakimu Kamugisha alitaka Lema kudhaminiwa na wadhamini wawili wanaotambulika kwa dhamana ya Sh10 milioni kila mmoja, pia hati yake ya kusafiria ikabidhiwe mahakamani na hataruhusiwa kusafiri nje ya nchi bila ruhusa ya Mahakama katika kosa la kwanza.
Katika shtaka la pili alimtaka Lema kudhaminiwa na watu wawili wanaoamilika kwa dhamana ya Sh15 milioni kila mmoja na pia alitakiwa kukabidhi hati ya kusafiria na kutosafiri nje ya nchi bila kibali cha Mahakama. Hata hivyo, wadhamini hao ambao ni madiwani Paul Matson na Aman Lewadi vitambulisho vyao vilitofautiana majina na kuwekewa pingamizi, hatua ambayo ilifanya hakimu kuwataka kwenda kurekebisha kasoro hizo.
Vurugu mahakamani
Wakati wadhamini hao wakisubiriwa ilipofika saa 8.27 mchana, polisi walitaka kumpeleka Lema mahabusu, hatua ambayo ilizua vurugu baada ya mbunge huyo kupinga kwa kuwa muda wa mahakama ulikuwa haujaisha.
“Mtaniua hapa, siendi magereza, polisi mtaniua hapa siendi, muda wa mahakama bado haujaisha na wadhamini wangu wapo njiani wanakuja,” alisikika Lema.
Kutokana na vurugu hizo, Lema alikimbia na kuingia mahakamani, hatua ambayo ilisababisha vurugu hadi pale maofisa wa Mahakama walipoingilia kati na kueleza kuwa mtuhumiwa huyo anasubiri kudhaminiwa na wadhamini wake walikuwa wamefika.
Ilipofika saa 10.47 jioni Lema alikamilisha dhamana yake na kuachwa na alitolewa mahakamani akiwa amebebwa na baadhi ya madiwani na wafuasi wa Chadema.
Akizungumza na mahakamani hapo, Meya wa Jiji la Arusha, Kalisti Lazaro alisema hali ya Lema ni mbaya na kwamba alipelekwa moja kwa moja Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu.
Akizungumza akiwa hospitalini, Lema alisema ameshangazwa na yaliyotokea tangu kukamatwa hadi mahakamani.
Adai alifunga, hakugoma kula
Alisema aligoma kula tangu Ijumaa hadi jana asubuhi kutokana na kuamua kufunga kwa ajili ya Taifa.
“Hali ni mbaya kwa sasa, sikula siku tatu kutokana na kuliombea Taifa amani na utulivu,” alisema.
Baraza laahirishwa
Kikao cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Arusha, kiliahirishwa jana na Kaimu Mkurugenzi, Anna Mwambene kutokana na madiwani wengi kwenda mahakamani kusikiliza kesi ya Lema na hivyo akidi kushindwa kutimia. Madiwani 14 kati ya 36 ndiyo waliokuwa ukumbini na Meya Lazaro alisema wengine licha ya kutokwenda mahakamani wamejificha kutokana na kusakwa na polisi kwa tuhuma za kuchochea maandamano ya Septemba Mosi.
Imeandikwa na Mussa Juma, Zulfa Mussa na Filbert Rweyemamu.
Mwananchi.
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT