Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Johnson Minja alisema Serikali ni kusogeza huduma kwa wananchi walio wengi kwa kuwa Dodoma iko katikati ya nchi.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Minja alisema katika kipindi hiki cha mpito, kuna fursa nyingi ambazo zimejitokeza kufuatia uamuzi huo wa Serikali. Alisema kutakuwa na uhitaji mkubwa katika sekta ya ujenzi na hata samani za nyumbani na ofisini.
Minja alifafanua kuwa Serikali ikihamia Dodoma itarahisisha mchakato wa biashara hasa kwa wafanyabiashara wa mikoa ya kusini. Anatoa mfano kwamba kama mfanyabiashara anatumia siku mbili kwenda Dar es Salaam kupata huduma, sasa atatumia muda mfupi kupata huduma hizo Dodoma na kurudi mkoani kwake.
“Changamoto kwetu itakuwa ni kasi ya Serikali kujenga miundombinu, lakini wafanyabiashara wako tayari. Serikali ikichelewa kuweka miundombinu kama maji na barabara, wafanyabiashara nao watashindwa kwenda kasi katika uwekezaji wao,” alisema Minja.
Minja alisisitiza kwamba jiji la Dar es Salaam litaendelea kuwa kitovu cha biashara nchini kwa sababu kuna bandari. Anasema bandari ndiyo lango la kibiashara ambalo linafungua soko la bidhaa zinazokwenda bara.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa reli ya kisasa kutafungua zaidi kasi ya biashara na mji wa Dodoma. Alisema bandari na reli vinategemeana, kwa hiyo Dodoma ikiwa na reli ya kisasa itapokea mizigo kutoka bandarini kwa haraka.
“Tusijiunge na walalamikaji, tuangalie fursa ili tukuze uchumi wetu binafsi na Taifa kwa ujumla. Suala la biashara ni tofauti na siasa, nawashauri wafanyabiashara wenzangu tujiweke mbali na siasa, tuangalie fursa za kibiashara,” Minja aliwashauri wafanyabiashara.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicholas Mgaya alisema Dodoma ni mji utakaokua kwa kasi na fursa ndiyo zinavyoongezeka. Aliwataka wananchi kuchangamkia fursa hizo.
“Uamuzi wa kwenda Dodoma ni wa siku nyingi, hatushangai kwa hilo. Ni wazi kuwa hatua hiyo itafungua fursa nyingi za kibiashara na Dodoma itakuwa kwa kasi. Hatuhitaji kusukumwa ili kutumia fursa zilizopo,” alisema Mgaya.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEOs - Roundtable), Ali Mufuruki anasema Serikali ikihamia Dodoma wafanyakazi wataongezeka katika mji huo, hivyo mahitaji ya nyumba yatakuwa makubwa.
Alisema soko la bidhaa mbalimbali litaongezeka pia ili kukidhi mahitaji ya watu hao. Alisema kwa muda mrefu Dodoma imekuwa soko la msimu hasa wakati wa Bunge, hivyo wafanyabishara walikuwa na hofu ya kuwekeza katika mji huo.
“Watumishi wa Serikali wakihamia Dodoma watahitaji makazi, shule nzuri kwa ajili ya watoto wao, hospitali na hoteli kwa ajili ya wageni watakaotembelea mji huo. Zote hizo ni fursa kwetu wafanyabiashara,” alisema Mufuruki.
Mfanyabiashara huyo alisema Serikali ikihamia Dodoma itatoa fursa nyingine kwa jiji la Dar es Salaam kupangiliwa vizuri na kubaki mji wa kibiashara. Anasema sekta binafsi itapata nafasi kubwa Dar es Salaam kwa sababu Serikali itauza majengo yake yote.
Alizitaka halmashauri za jiji la Dar es Salaam kuandaa mipango miji mizuri ili mji uwe na sura nzuri. Anasema Serikali ilishindwa kuupangilia vizuri mji wa Dar es Salaam kwa sababu mipango miji yake ni ya kizamani na idadi ya watu inakuongezeka kila uchao, mbali na wanaozaliwa pia wapo wanaotoka vijijini nan je ya mkoa wa Dar es Salaam wanaokuja mjini kutafuta maisha.
Mufuruki alibainisha kwamba watu wanaweza kuchukua mikopo benki ili kutekeleza mipango ya kibiashara kulingana na fursa walizoziona. Anasema mtu mwenye dhamira ya kweli ataweza kufanya biashara vizuri na kurejesha mkopo ndani ya muda mfupi.
“Serikali iweke wazi mipango yake ili watu wajue kwamba wakichukua mkopo benki, nini watakachofanya cha uwekezaji na uzalishaji. Siyo watu wanachukua mkopo leo halafu kesho Serikali inasema imeahirisha kwenda Dodoma. Ni muhimu mambo yote yakawekwa wazi na kutekelezwa ilivyopangwa,” alisema Mufuruki.
Mtaalamu wa masuala ya maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa Benedict Mongula alisema Serikali haitawasukuma watu kukimbilia fursa katika mji wa Dodoma, bali wenye maono makubwa watakwenda wenyewe.
Anasema soko la Dodoma litaongezeka na kuruhusu soko la Dar es Salaam kupumua kidogo. Anasema changamoto katika mchakato wa Serikali kuhamia Dodoma ni fedha za kugharamia mchakato huo.
“Serikali ikihamia Dodoma watu watakwenda wenyewe kufanya biashara. Baada ya muda mfupi tutaona kila kitu kikipatikana kule. Uwekezaji mkubwa kama nyumba utachukua muda kidogo,” alisema Profesa Mongula.
Alisisitiza kwamba katika uchumi huria, soko linajitengeneza lenyewe bila hata Serikali kuingilia kati. Anasema hatua ya Serikali kuhamia Dodoma itawanufaisha watu kutoka kona mbalimbali za nchi hii.
“Licha ya changamoto zinazoikabili Serikali katika kutekeleza mpango huo, wafanyabiashara wanatakiwa kuangalia fursa za kibiashara. Shughuli za kibiashara na uzalishaji ndiyo zitakazorahisisha mchakato huo kukamilika kwa wakati kupitia makusanyo ya kodi,” alisema Profesa Mongula.
Chanzo:Gazeti la Mwananchi.
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT