KUELEKEA DODOMA: Dodoma inazo fursa muhimu zipo hapa. | bongo satellite.
Breaking News
Loading...

Monday, 15 August 2016

KUELEKEA DODOMA: Dodoma inazo fursa muhimu zipo hapa.

DOM
Baada ya Rais John Magufuli kutangaza nia ya Serikali kuhamishia makao makuu Dodoma, watu wamekuwa wakiutazama mkoa huo kwa jicho la fursa za kiuchumi zaidi.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa alitangaza kuhamia mkoani humo ifikapo Septemba mwaka huu. Kuhamia kwake kutatanguliwa na mawaziri walio chini ya ofisi yake na wengine.
Licha mawaziri, naibu mawaziri kuwa na ofisi zao jijini Dar es Salaam, huwa wana makazi na ofisi zao ndogo Dodoma. Hivyo sasa watahamia rasmi wakifuata makatibu wakuu na wakurugenzi wa idara zao na watumishi wengine wa makao makuu. Inakadiriwa kuwa watumishi zaidi ya 100,000 watahamia Dodoma.
Idadi hiyo inatarajiwa kuongeza fursa za biashara kwa mkoa huo na mikoa ya jirani.
Miongoni mwa fursa za biashara zinazojitokeza mkoani humo ni ufugaji wa nyuki na biashara ya asali. Dodoma huzalisha tani zaidi ya tano za asali kwa mwaka, lakini mahitaji ya mkoa huo ni tani sita, hivyo uzalishaji huo hautoshi.
Mwakilishi wa chama cha ushirika wa wafugaji nyuki, Peter Mwaluko anasema makao makuu yakihamia Dodoma yatawasababisha wafuga nyuki kutafakari upya soko lao la asali.
“Tumekuwa tukitoa mafunzo kwa wafugaji wa nyuki, kutoa vifaa vya kufugia na masoko ya asali. Kwa sasa tunazalisha tani zaidi ya tano kwa mwaka ambazo hazitoshi hata kwa mkoa wenyewe. Kwa hiyo tuna changamoto kubwa ya uzalishaji hafifu,” anasema Mwaluko.
“Kwa hapa Dodoma mjini tuna vijiji 10 vyenye wafugaji tunaowahudumia. Wilaya nyingine kuna wastani wa vijiji 20 kila wilaya ambao pia tunawahudumia. Kikubwa tunachofanya ni kuwahimiza kutunza mazingira kwa kutokata miti hovyo ili nyuki wapate mazingira mazuri ya kuzalisha sukari,” anasema Mwaluko.
Anasema ili kukabiliana na soko kubwa linaloongezeka, wanashirikiana na ushirika mpya wa wafuga nyuki na kuomba msaada wa fedha kutoka serikalini ili kusaidia uzalishaji.
“Kwa sasa tunategemea fedha kwa wafadhili kutoka nje ya nchi, lakini tunaiomba Serikali itusaidie ili tukabiliane na soko kubwa linaloendelea kuongezeka,” anasema Mwaluko.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, mhadhiri wa shule kuu ya biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Omar Mbula wa anasema uhamisho huo utapanua wigo wa biashara katika mkoa huo.
“Kuna nadharia moja inayoongelewa kwenye ujasiriamali kwamba kukiwa na matatizo watu huwa wabunifu zaidi katika kuangalia nini kifanyike ili wafanye vizuri zaidi, kinachofanyika kwa sasa ni kwamba, mianya ya kibiashara iliyokuwapo Dodoma, itajitokeza kwa urahisi zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzo,” anasema Dk Mbula.
Anasema miongoni mwa njia za kuongeza soko ni ongezeko la watu katika eneo husika na watu hao wawe na uwezo wa kununua bidhaa.
“Kuna njia za kuimarisha soko, moja ni kuwa na watu, lakini watu hao ni wa aina gani? Kwa kuhamishia watumishi wa Serikali Dodoma maana yake ni kwamba tutakuwa na watu wenye kipato cha kati na cha juu. Hiyo itawezesha, wafanyabiashara kuiona mianya ya biashara kuliko ilivyokuwa mwanzo,” anasema.
Kwa Dar es salaam, anasema kuna athari zitakazojitokeza kwa sababu baadhi ya shughuli zilizokuwa hapo kwa kiasi kikubwa zitahamia Dodoma na kutakuwa na mianya mikubwa hapo na maeneo yaliyo karibu.
“Kwa mfano kwa sasa bei ya viwanja Dodoma imeshaanza kupanda. Lakini itawawezesha wale walioko Dar es Salaam wawe na mbinu za kutumia zile mali walizonazo kwa mianya mingine ambayo haitokani na Serikali moja kwa moja,” anasema Dk Mbula.
Hivi karibuni, Taasisi ya sekta binafsi (TSPF) imetangaza kupokea kwa mikono miwili uamuzi wa Serikali kuhamishia makao yake makuu Dodoma.
Mkurugenzi wa TSPF, Godfrey Simbeye alisema hivi karibuni kuwa huo utakuwa mkakati wa kusukuma mbele uimarishwaji wa sekta ya viwanda, biashara na kuondoa msongamano  jijini Dar es Salaam.
“Sekta binafsi inaona nia ya Serikali kuhamia Dodoma kama fursa muhimu kwa sababu uwekezaji mwingi utahitajika ili kukidhi idadi ya watu watakaokuwapo,” alisema Simbeye.
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT